Mfano wa Ngano, Vigano, Soga, Tarihi na Visakale

Sungura akitembea

Maana ya hadithi

Awali ya yote, nitatoa maana ya hadithi kama ninavyoelewa mwenyewe katika fikra zangu… Hadithi ni masimulizi yanayowasilishwa kwa lugha ya nathari kuhusu watu, wanyama na kitu chochote kile kinachoelezeka.
Kuna vipera vingi vya hadithi, ila vinavyoonekana kutambulika napengine kufundishwa zaidi ni: Ngano, vigano, soga, tarihi na visakale.
Lengo la mada hii ni kutoa mfano wa kila kipera kati ya vipera hivyo vingi. Uko tayari kutazama mifano hii? Kama jibu ni ndiyo, endelea kusoma.

Mfano wa ngano

Upo utata wa kitaaluma katika kutoa maana ya ngano, kwani wengine husema ngano ndiyo hadithi, japo sikubaliani nao, naamini wana haki ya kusema hivyo - midomo ikikosa cha kutafuna, hufyatua maneno! Maana yangu, huenda ikautoa utata huo, ama ikauendeleza. Ngano ni utungo wenye visa vya kubuni ambao wahusika wake huwa ni wanyama.
Hivyo unapoandika ngano, zingatia mambo haya:
Hadithi yako iwe na wahusika wanyama.
Iwe na funzo fulani.
Iwe na mwanzo maalumu: Kwa mfano, paukwa… pakawa.
Iwe na mwisho maalumu: kwa mfano, wakaishi raha msitarehe.
Sasa tazama mfano huu wa ngano…
MKASA WA SUNGURA NA FISI
Paukwaaa… Pakawaaaa
Hapo zamani za kale, Sungura na Fisi walikuwa marafiki walioshibana kwelikweli. Walipendana hata wakaamua kujenga kibanda ambao wao walikiita nyumba na wakaishi humo pamoja.
Siku moja Tembo alitembelea maeneo yao, hakukuwa na dalili ya amani kutembelewa na Tembo kwani alipofika tu, alikipiga teke kibanda chao, nacho kikatii kwa kuvunjika vipandevipande.
Fisi alijaribu kumzuia Tembo asiendelee kufanya uharibifu zaidi. Looh, aliambulia kuvunjwa mbavu mbili za kushoto. Sungura alijaribu kuhoji kwa nini Tembo alimvunja mbavu Fisi. Afanaleki, aliambulika kung’olewa meno matatu.
Basi Tembo aliporidhishwa na fujo zake mwenyewe, akaondoka zake kwa mwendo wa maringo. Sungura na Fisi, walijizoazoa na kujiganga.
Baada ya siku tatu, walikijenga tena kibanda chao. Safari hii, walitumia mbao imara kutoka msitu wa Mukula. Fahari ya macho, kibanda kilipendeza kikavutia viumbe wote wa msituni.
Ili kuepusha kuvamiwa tena na tembo, walitegesha utelezi katika njia ya kuja kwao. Tembo alipata taarifa za mtego huo, hivyo hakuthubutu tena kuwafuata. Sungura na Fisi wakaishi raha msitarehe.

Mfano wa vigano/kigano

Vigano ni hadithi ambazo hutumia methali katika kutoa mafunzo yake. Hadithi nzima hukitwa katika methali fulani ambayo ndiyo hasa hulenga kuleta ujumbe.
Tazama mfano wa kigano:
ASIYESIKIA LA MKUU HUVUNJIKA GUU
Mzee Mwinyi alimshauri kijana wake Hamidu asiwe na tamaa kwa kutamani vya watu. Siku zote alimuusia ya kwamba, tamaa ni mbaya na mwisho wake ni majuto.
Ilitokea siku moja, Hamidu akamuaga baba yake juu ya safari yake ya kwenda kijiji jirani. Baba yake alimuuliza mwanae ni nini alitaka kwenda kufanya huko. Hamidu alijibu kulikuwa na sherehe ya rafiki yake ambaye angepata jiko siku tatu zijazo.
Mzee Mwinyi alimruhusu Hamidu aende katika sherehe lakini akamkumbusha kuwa, asitamani vya watu. Naye Hamidu alikubali na kuondoka zake.
Kumbe Hamidu alidanganya, hakwenda katika sherehe, bali aliungana na marafiki zake wanne, wakaenda mjini kwa lengo la kuvamia duka la Mpemba mmoja aliyependwa sana na watu kwa sababu ya ukarimu wake.
Walifika mjini, wakapanga mkakati, kisha wakavamia katika duka usiku wa manane. Wakiendelea kupora mali, wapita njia walishtuka kuona hali isiyokuwa ya kawaida katika duka lile. Hatimaye waligundua uwepo wa wezi, ndipo wakapiga kelele.
Watu walijaa, Hamidu na wenzake walipigwa sana. Isingekuwa uwepo wa askari wa doria usiku ule, Hamidu na wenzake wangeuawa. Wakiendelea kuvuja damu, walichukuliwa mpaka kituo kidogo cha polisi. Huko walipatiwa huduma ya kwanza kisha wakawekwa rumande.
Hamidu akiwa rumande, alilia sana, alikumbuka ushauri wa baba yake, akajuta kwa jinsi alivyoupuuzia ushauri ule mzuri. Alipogundua kuwa hata meno yake manne ya mbele aliyapoteza, kilio kilizidi tena kikiwa na kwikwi nyingi.
Askari mmoja alimsogelea Hamidu na kumwambia, “Wewe ni kijana mdogo sana. Bila shaka hukusikiliza ushauri wa wazazi wako, siku zote, asiyesikia la mkuu huvunjika guu.”

Mfano wa visasili

Visasili ni aina ya hadithi ambazo huzungumzia asili ya vitu na mambo mbalimbali katika namna ya kufikirika tu. Tunaweza kusema, hadithi hizi, hubeba visa vya asili.
Tazama mfano wa kisasili:
SABABU YA MBUZI KUWA NA MKIA MFUPI
Hapo zamani za kale mbuzi na kondoo walikuwa marafiki. Waliishi pamoja katika nyumba yao iliyokuwa pembezoni kidogo mwa mji. Walipendana na walishirikiana kazi mbalimbali.
Mbuzi alikuwa na mkia mrefu kama wa ng’ombe. Aliupenda mkia wake kwa sababu ulimsaidia kufukuza nzi na wadudu wengine wasumbufu. Kondoo alikuwa na mkia mnene ulionona mafuta.
Kila walipotaka kupika wali, kondoo aliweka sufuria juu ya moto, sufuria likipata moto, anaweka mkia wake na kutoa mafuta wakapata kupika.
Mbuzi hakufurahia kuona kila siku rafiki yake ndiye anayetoa mafuta. Akaamua kumsaidia. Siku hiyo, mbuzi aliweka sufuria juu ya moto. Sufuria lilipopata moto na kuwa jekundu, mbuzi aliweka mkia wake. Loooh! Mkia ulinasa, hapohapo mbuzi akakimbia kuelekea mtoni ambako alitumbukia ndani ya maji na kufanikiwa kuuzima moto ule. Hata hivyo, mkia wa mbuzi uliungua vibaya na kufanya kibaki kipande kidogo kama tukionacho leo.

Hiyo ndiyo sababu ya mbuzi kuwa na mkia mfupi.

Mfano wa Tarihi

Tarihi au visakale ni hadithi ambazo husimuliwa kuhusu matukio ya kihistoria. Simulizi hizi mara nyingi, hutia chumvi katika matukio ya kihistoria na kuyafanya yawe nusu ukweli nusu uongo.
Sasa tazama mfano wa tarihi:
SHUJAA MKWAWA
Mkwawa kiongozi wa wahehe, ni shujaa. Ushujaa wake umejengwa katika namna alivyoweza kuwashikisha adabu wote walioitakiwa mabaya jamii yake. Inasemekana, ufalme wake aliurithi kutoka kwa baba yake.
Mwaka fulani katika kipindi cha utawala wa Mkwawa, Wajerumani walitua katika jamii yake na kumtaka atoke. Mkwawa alikataa na kuamua kuanzisha vita ili kuwatetea watu wake. Mkwawa hakuwaogopa wazungu na mianzi yao.
Vita vilikuwa vikali, Wajerumani walipigwa vibaya wakakimbia. Shujaa Mkwawa aliweza kuteka siraha zao za kivita. Pia shujaa huyu aliweza kumuua kamanda wa jeshi la Wajerumani aliyeitwa Zelewiski.

Wajerumani walipokimbia, waliahidi kuwa, wangekwenda nyumbani kwao kujifunza mbinu alizotumia Mkwawa kuwapiga kisha wangerejea kumshikisha adabu. Mkwawa hakujali, shujaa huyu hakuogopa lolote!

Mfano wa soga

Soga ni hadithi zenye ucheshi ndani yake. Hadithi hizi zisimuliwapo, usipocheka basi utatabasamu.
Sasa tazama mfano wa soga:
ABUNUWASI NA MTEJA WAKE
Abunuwasi alikuwa fundi cherehani mashuhuri katika nchi ya Baghdad. Alisifika kila kona ya nchi hata sifa zake zikavuka mipaka ya nchi yake.
Siku moja Abunuwasi akiwa katika shughuli zake za kushona nguo za wateja, alipokea mteja mpya aliyevalia mavazi ya gharama. Baada ya salamu, mteja akaeleza mahitaji yake.
“Fundi nishonee nguo ambayo si nyeusi, nyeupe, kijani… kwa ufupi ni kwamba, nishonee nguo ambayo haina rangi yoyote!”
Abunuwasi alimtazama mteja wake usoni. Kisha kwa sauti tulivu akajibu.
“Nimekusikia mteja wangu, nitakushonea nguo uitakayo, hata hivyo, usiifuate nguo hii Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Alhamisi, Ijumaa, Jumamosi, Jumapili… Kwa ufupi ni kwamba, usiifuate siku yoyote.

Mteja mpya, aliinamisha kichwa chake chini kwa haya kisha akaondoka zake kurejea alikotoka. Watu wa Baghdad waliposikia habari hii, walimpongeza Abunuwasi kwa maarifa yake huku wakicheka.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne