Uhuru wa Mwandishi wa Kazi za Fasihi Dhidi ya Tabaka Tawala

UHURU WA MWANDISHI WA KAZI ZA FASIHI

Uhuru wa mwandishi ni hali ya mwandishi kuwa huru katika uandishi wa kazi zake.

Kuna uhuru wa mwandishi?

Uhuru wa mwandishi huamliwa na tabaka tawala. Mwandishi anapojaribu kulisema tabaka tawala huenda akanyanyaswa na kufungiwa kwa kazi zake. Endapo ataamua kuwa kasuku kwa kupongeza kila kinachofanywa na watawala, kazi zake zitapongezwa na kupigiwa debe.
Ipo mifano mingi ya waandishi ambao kazi zao zilipigwa marufuku baada ya kulisema bila woga tabaka tawala. Tamthiliya ya ‘I Will Marry When I Want’ ya Ngugi Wa Thion’go ilikumbana uso kwa uso na rungu la mdhibiti baada ya kulisema tabaka tawala.
Rosa Mistika ya Kezilahabi nayo ilifungiwa na mdhibiti kwa sababu watumishi wa serikali walisemwa waziwazi.
Huko Afrika ya Kusini, nguvu kupita kiasi zilitumika dhidi ya waandishi ambao walikwenda kinyume na tabaka tawala. Waandishi hao walinyanyaswa mpaka wakahama nchi yao.
Mwaka 1975 na 1976, vitabu vyote vya David Mailu vilipigwa marufuku nchini kwa madai kuwa, vilieleza mambo ya aibu waziwazi. Ilikuwa ni ajabu mno kuzuiwa kwa vitabu hivi na kuachwa vitabu kama ‘Kama Sutra’ vilivyozungumzia masuala ya ngono bila kificho.
Kutokana na watawala kutopenda kusemwa waziwazi, mbinu ya waandishi wengi imebadilika na kuwa ile ya kutumia mafumbo kwa lengo la kukwepa udhibiti wa kazi zao.
Kezilahabi baada ya riwaya yake kufungiwa kwa sababu zisizoeleweka, alimua kuja na mtindo mpya katika riwaya zake mbili, Nagona na Mzingile. Katika riwaya hizo, ametumia mtindo wa uandishi ambao umejaa mafumbo na si rahisi kuelewa kilichoandikwa hasa maana yake nini?

Faida ya mwandishi kuwa huru

i.             Mwandishi atakuwa huru kuikosoa jamii yake na tabaka tawala bila woga. Mwandishi atakuwa huru kuonyesha maovu yote yanayotendeka katika jamii.
ii.            Mwandishi atakuwa na msimamo. Msimamo huu utaendana  na kuwa na falsafa moja inayoeleweka na kumwepusha na uandishi wa kutazama watawala wanataka nini!
iii.           Unafiki na ukasuku wa waandishi utakwisha. Mwandishi ambaye hana uhuru wake hugeuka kasuku wa watawala. Hujipendekeza na kujikomba kwao ili kumwepusha na rabsha za watawala.

iv.          Fasihi inakuwa chombo cha kuikomboa jamii. Lengo la fasihi ni kuleta ukombozi katika jamii. Mwandishi huru ni nyenzo muhimu katika kuifikia jamii imara.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie