Nadharia Mbalimbali Zinazoeleza Maana ya Fasihi
Tunapouliza maana ya fasihi,
tunakutana na maana nyingi kinzani. Maana yake ni kwamba kila mmoja aliifasiri
fasihi kwa mtazamo wake. Kutokana na maana hizo kuwa nyingi na kutofautiana,
kundi la nadharia hizi lilionekana kuwa na nguvu na ushawishi kiasi juu ya nini
hasa maana ya fasihi.
Nadharia mbalimbali zinazojaribu kueleza maana ya fasihi ni:
1. fasihi ni kioo
Maana yake ni kwamba, fasihi ni kioo ambacho mtu anaweza
akajitazama na kuona taswira yake.
Nadharia hii inakumbana na
changamoto mbili:
Kwanza, kioo hakiwezi kumweleza
mtu ni wapi anatakiwa ajirekebishe.
Pili, huwezi ukajiona sehemu zote
katika kioo.
2. Fasihi ni hisi
Hii ina maana kwamba, ni lazima
mwandishi au mhusika wa kazi yoyote ya fasihi apate mguso fulani ndipo aweze
kuandika au kuitoa kazi yake.
Nadharia hii inaibua maswali
mengi. Je ni lazima mtunzi wa kazi ya fasihi aguswe ndipo aweze kutoa kazi
yake? Bila hisi hakuna kazi ya fasihi? Waandishi wa kazi za fasihi kama Penina
Mhando, Kezilahabi, Shaaban Robert na wengineo waliguswa mara ngapi? Maswali
haya yanakosa majibu hivyo nadharia hii haijitoshelezi.
3. Fasihi ni mwamvuli
Kama ambavyo mwamvuli huweza
kumkinga mtu dhidi ya mvua na jua kali, ndivyo fasihi ilivyo na uwezo wa
kuzikinga amali za jamii zisiharibike.
Hata hivyo nadharia hii inakosa
mashiko kwani jamii hubadilika mara kwa mara. Mfano zipo mila na desturi
zilizohifadhiwa na makabila mengi na hazina nafasi hii leo. Hivyo, mwamvuli
utatoboka kwani hautaweza kuhimili vishindo vya mabadiliko yanayotokea katika
jamii.
4. Fasihi ni Sanaa ya Uchambuzi wa Lugha Inavyosemwa,
Inavyoandikwa na Kusomwa
Maana hii ina ukweli kwa kiasi
fulani kwani ni kweli fasihi msingi wake mkubwa ni lugha na hakuna kazi ya
fasihi bila lugha. Hata hivyo si kweli kwamba, fasihi inahusu uchambuzi wa lugha
pekee, vipo vipengele vingi kama, dhamira, ujumbe, migogoro, wahusika na
vipengele vingine kadha wa kadha.
Nini maana ya fasihi?
Baada ya kutazama nadharia hizo,
sasa tutazame maana ya fasihi ambayo inaelekea kukubalika.
Fasihi ni sanaa inayotumia lugha
katika kufikisha ujumbe wake. Fasihi huipa jamii maarifa na mbinu za kupambana
na mazingira ili kuondoa uozo katika jamii kwa lengo la kuleta haki na
maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Marejeo:
Nkwera, F. (1978) Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo. TPH:
Dar es Salaam.