Past Paper | Mtihani wa Kiswahili | Kidato cha Nne 2011

PAST PAPER: MTIHANI WA KISWAHILI:  KIDATO CHA NNE 2011

SEHEMU A (Alama 10)

UFAHAMU

Jibu maswali yote​ katika sehemu hii.

1.    Soma kwa makini kifungu cha habari kifuatacho kisha jibu maswali yanayofuata: Misitu ya nchi ni mingi sana hata wakati mwingine tunadanganyika kuwa haitakwisha kamwe. Tunaamini kwamba tunaweza kuendelea kuitumia miti yake na kuikata kwa ajili ya kupata mashamba na malisho ya wanyama wetu bila kujishughulisha kupanda au kuhifadhi mingine kwa ajili ya siku za mbele.
Fikiria tulivyo na mawazo potofu. Fikira mbaya kama hizo wanazo watu wengi nchini mwetu. Kwa hiyo imenilazimu kuwaonesheni kuwa misitu ni lazima ilindwe na haitalindwa kwa manufaa ya kizazi chetu cha sasa tu, bali pia kwa ajili ya vizazi vyetu vijavyo.
Basi mjue kuwa kama misitu yote itakatwa patakuwa na upungufu mkubwa wa mbao na pia upungufu wa maji ambao ni mbaya zaidi. Ubaya kama huu hautakiwi utokee katika Taifa letu linalosonga mbele. Hatuwezi kuruhusu uharibifu wa misitu yetu uendelee kufanyika kwa sababu unarudisha nyuma hali ya maisha yetu na unazuia ustawi wa nchi yetu.
Hebu fikiria kwanza maisha yetu yatakuwaje iwapo miti itakosekana - taabu ya kupika, gharama ya kujenga kwa chuma, mawe au udongo ulaya badala ya miti. Gharama ya viti, vitanda na meza ikiwa vitatengenezwa kwa chuma tu. Halafu fikiria kama maji yote yakikauka, ninyi nyote mwajua shida zitakazotokea, kwa hiyo hatutaki kabisa shida kutokea.
Kwa nini tuwe na shida ya kukosa maji katika sehemu ambazo zina maji ya kutosha? Basi inatupasa kuona kwamba kuna ulazima wa kuhifadhi misitu kwa ajili ya matumizi ya leo na kesho.
Bila shaka sasa utajiuliza mwenyewe. Je, siwezi kukata kabisa misitu ili niweze kulima? Jibu ni kwamba unaweza kabisa, lakini ni katika sehemu zile ambazo hazikuhifadhiwa. Tena ifahamike kwamba sehemu ambazo zimehifadhiwa ni chache sana ukilinganisha na mapori makubwa yaliyobaki wazi kwa ajili ya kilimo. Sasa nataka kusisitiza hasa juu ya misitu iliyohifadhiwa.
Hizi ndizo sehemu za misitu ambazo ni za lazima sana, na inatakiwa zihifadhiwe daima kwa matumizi ya faida ya Taifa. Misitu iliyohifadhiwa ni misitu inayotazamiwa kudumu daima nchini. Inatunzwa ili itumiwe kwa utaratibu ulio bora kwa kizazi hata kizazi.
Kwa wakati ujao misitu hiyo itatoa mbao za kujenga nyumba, shule, hospitali na majengo mengine, pia kutengeneza viti, meza, makabati, milango, madirisha na masanduku. Hata sasa, mbao nyingi zitumikazo hutokana na miti iliyoota katika misitu iliyohifadhiwa.
Lakini kwa sababu ardhi yenye misitu ya aina hiyo inahitajiwa sana kwa kilimo, itatubidi kuanza kuotesha misitu mipya kwa ajili ya mahitaji yetu. Basi ni lazima niwakumbushe wananchi kuwa miti iliyomo katika misitu iliyohifadhiwa haitatosha kufanyia kazi zetu zote ili kuinua maisha ya watu na kuinua uchumi wa nchi.
Misitu iliyohifadhiwa lazima iongezwe kwa kupanda miti mingine, kwa mfano hivi sasa Idara ya misitu inapanda miti kati ya eka elfu nne na tano kila mwaka na pia inaangalia miti ya asili katika sehemu kubwa kabisa ya nchi hii.

Maswali

(a) Kwa mujibu wa habari uliyosoma watu wengi hufikiria nini juu ya misitu?
(b) Mwandishi wa habari hii anasema ni jambo gani huleta uharibifu wa misitu?
(c) Mwandishi anashauri misitu ikatwe katika sehemu gani?
(d) Je, ni madhara gani yatatokea endapo misitu itatoweka kabisa?
(e) Je, ni sahihi kusema kuwa kwa vile kuna misitu iliyohifadhiwa hakuna haja ya kushughulika na kupanda miti nchini? Kwa nini? 2.
2. Fupisha aya tatu (3) za mwisho za habari uliyosoma kwa maneno themanini (80).

SEHEMU B (Alama 25)

SARUFI NA UTUMIZI WA LUGHA

Jibu maswali yote​ katika sehemu hii.
3. Tumia kiambishi “KA” kuonesha matukio kumi (10).
 4. “Kila lugha ina tabia ya kuchukua maneno kutoka lugha nyingine ili kukidhi mahitaji yake kimsamiati.” Fafanua kauli hii ukitumia maneno kumi (10) ya Kiswahili.
5. Yapange maneno yafuatayo kama yanavyoonekana katika kamusi, kisha eleza maana ya kila neno kwa kutoa mfano mmoja (1) wa sentensi.
(a) Falsafa (b) Barizi (c) Anuwai(d) Barubaru (e) Kinda (f) Ajuza (g) Fanusi (h) Ghaibu (i) Goigoi (j) Kinanda
6. Eleza maana ya upatanisho wa kisarufi. Fafanua jibu lako kwa kutoa mifano minne.
7. “Misemo mingi hutumika kwa madhumuni ya kulinda heshima na kuvuta makini ya watu.” Fafanua usemi huu kwa kutumia misemo mitano (5).

SEHEMU C (Alama 10)

UANDISHI Jibu swali moja (1)​ kutoka sehemu hii.

8. Andika insha isiyo ya kisanaa yenye maneno mia mbili na hamsini (250) kuhusu mandhari ya shule yenu.
9. Andika kumbukumbu za kikao cha wanafunzi kuhusu sherehe ya kumuaga mkuu wenu wa shule aliyepata wadhifa wa kuwa Afisa Elimu wa Mkoa.

 SEHEMU D (Alama 10)

MAENDELEO YA KISWAHILI

Jibu swali la kumi (10)

10. Fafanua athari ya Waarabu katika lugha ya Kiswahili kwa kutoa hoja nne (4).

SEHEMU E (Alama 45)

FASIHI KWA UJUMLA

Jibu maswali matatu (3)​ kutoka katika sehemu hii. Swali la 15 ​ni la lazima.

11. Sifa muhimu mojawapo ya methali ni kujenga picha au taswira ambazo huchotwa katika mazingira yanayoizunguka jamii.” Thibitisha hoja hii kwa kutumia methali tano (5).
12. “Maelekezo yanayotolewa na msanii wa fasihi hukidhi matarajio ya jamii yake.” Kwa kutoa hoja tatu (3) kwa kila mchairi, jadili kauli hii kwa kuwatumia washairi wawili (2) kati ya walioorodheshwa.
13. “Nyimbo ni mbinu ya kifani ambayo wasanii wengi huitumia ili kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa hadhira.” Thibitisha usemi huu kwa kutumia waandishi wawili (2) wa riwaya kati ya waliorodheshwa.
14. Jadili jinsi wasanii wawili (2) wa tamthiliya mbili (2) ulizosoma walivyotumia mbinu ya kicheko kutoa ujumbe walioukusudia kwa jamii.
15. Eleza muundo wa soga. Tunga soga ya kusisimua kuhusu kisa cha kubuni.

ORODHA YA VITABU

Ushairi Wasakatonge - M.S. Khatibu (DUP)
Malenga wapya - TAKILUKI (DUP)
Mashairi ya Chekacheka - T.A. Mvungi (EP & D. LTD)
 Riwaya Takadini - Ben Hanson (MBS)
Watoto wa Mama N’tilie - E. Mbogo (H.P)
Joka la Mdimu - A.J. Safari (H.P)
Tamthiliya Orodha - Steve Raynolds (MA)
Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe - E. Semzaba (ESC)
 Kilio Chetu - Medical Aid Foundation (TPH)

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie