Uhakiki wa Kazi za Fasihi Andishi | Kuuelewa Uhakiki

watoto wa mamantilie orodha na mashairi ya chekacheka


Uhakiki ni kitendo cha kutathimini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalumu.

Kwa maana nyingine tunaweza kusema, uhakiki ni uchambuzi wa kina wa kazi za fasihi kama vile riwaya, tamthiliya na mashairi kwa lengo la kufafanua vipengele vya fani na maudhui.

Misingi ya uhakiki

Misingi ya uhakiki hujikita katika fani na maudhui, nazo fani na maudhui huwa na vipengele vyake ambavyo ndivyo huhakikiwa.

Kuhakiki Fani

Fani ni mbinu anazotumia mwandishi ili kuwasilisha maudhui.

Vipengele vya fani ni;

i.              Mtindo

Mtindo ni mbinu za kipekee zinazotofautisha msanii mmoja na mwingine. Mambo yaonekanayo katika mtindo ni; matumizi ya monolojia, dayolojia, barua, nyimbo, nafsi n.k

ii.            Muundo

Ni mpangilio wa visa na matukio katika kazi ya fasihi. Miongoni mwa aina za uwasilishaji wa visa na matukio ni;

Muundo wa moja kwa moja au msago

Hii ni namna ya moja kwa moja ya kusimulia matukio, yaani kuanzia tukio la kwanza hadi la mwisho kwa namna yalivyotukia.

Muundo wa urejeshi

Huu ni usimuliaji wa kurukaruka hatua, yaani msimuliaji anaweza kuanzia katikati, akaja mwisho na kumalizia na mwanzo.

iii.           Wahusika

Wahusika ni watu au viumbe ambavyo mwandishi wa fasihi huwatumia ili kufikisha ujumbe kwa jamii husika.

Wahusika hugawanywa katika makundi mawili;

Wahusika wakuu

Ni wale ambao wanajitokeza kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa kazi ya fasihi.
Wahusika wadogo

Wahusika hawa hujitokeza mara chache na huwa na lengo la kumsaidia mhusika mkuu kufikisha ujumbe.

Wahusika hawa wawe ni wakuu au wadogo wanaweza kugawanyika katika makundi yafuatayo:

  1. Mhusika mviringo ni mhusika ambaye anabadilika kitabia na kimawazo kulingana na hali halisi ya maisha. Kwa mfano wanaweza kuanza kama watu wema lakini hali ya maisha ikawabadilisha na kuwa watu wabaya au wanaweza kuanza kama watu wabaya na hali ya maisha ikawabadilisha na kuwa watu wema.
  2. Mhusika bapa ni mhusika ambaye habadiliki kulingana na hali halisi ya maisha. Mfano; kama ni mwema basi atakuwa mwema kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho na kama ni mbaya basi atakuwa mbaya kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho.

iv.           Mandhari

Ni sehemu ambayo matukio ya kazi ya fasihi yanafanyika.

Matumizi ya lugha

Lugha ndiyo nyenzo kuu katika kazi ya fasihi, matumizi ya lugha hupita katika maeneo matatu;

1.    Tamathali za semi

2.    Misemo, methali na nahau

3.    Matumizi ya picha na taswira

Tamathali za semi

Tamathali za Usemi ni matumizi ya maneno kwa namna fulani ili kuifanya lugha iwe ya kuvutia na kuifanya kazi ya sanaa iwe ya kupendeza.

Baadhi ya tamathali za semi;

Tanakali za Sauti:Ni mbinu ya kutumia maneno yanayoiga sauti au hali fulani. Mfano ‘nyau’.

Tashibiha: Hii ni mbinu ya lugha inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti kwa kutumia maneno ya kulinganisha; ‘kama’, ‘mithili ya’, ‘sawa na’, ‘ja’. Mfano, ‘mnene kama kabati’.

Tashihisi: Hii ni mbinu ya kupatia kitu kisicho binadamu sifa ya mwanadamu. Mfano, ‘Panya akasema, “Nani atamfunga paka kengele.”

Takriri: Ni mbinu ya kurudiarudia neno moja au kifungu cha maneno ili kusisitiza ujumbe fulani. Mfano, alikimbia, alikimbia, alikimbia hadi akashika nafasi ya kwanza.

Sitiari: Ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili moja kwa moja kwa kutumia kiungo ‘ni’ ama ‘kuwa’. Mfano; Maisha ni mlima, Magwangwala ni mwamba.

Mubaalagha: Ni kutumia maneno yaliyotiliwa chumvi ili kusisitiza ujumbe fulani. Mfano. ‘Nina nguvu nyingi, nilimpiga kofi punda akakohoa.’

Kuhakiki Maudhui

Maudhui ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa katika kazi ya fasihi.

Vipengele vya maudhui ni pamoja na;

1.    Dhamira; hili ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Dhamira zimegawanyika katika makundi mawili, kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo.

2.    Migogoro; hii ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika, familia zao, matabaka yao, au hata katika nyadhifa mbalimbali. Vilevile migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii, migogoro ya nafsi, na migogoro ya kisiasa ambayo hujitokeza katika mitazamo tofauti kulingana na mtiririko wa visa na matukio yanavyopangwa na mwandishi.

3.    Ujumbe; hili ni funzo linalopatikana katika kazi ya fasihi.

4.    Msimamo; Msimamo ni ile hali ya mwandishi kuamua kufuata na kushikilia jambo fulani. Ama ni jinsi ambavyo mwandishi anatoa masuluhisho juu ya matatizo fulani katika jamii. Kuna aina mbili za msimamo,

-          Msimamo wa kiyakinifu/kimapinduzi; msimamo huu huyaangalia mambo kisayansi na hutoa masuluhisho yanayoweza kuondoa tatizo endapo yatafanyiwa kazi. Mfano suluhisho la umasikini wa nchi zinazoendelea ni kufanya kazi kwa bidii.

-          Msimamo wa kidhanifu; msimamo huu msingi wake mkuu ni mambo ya kudhani tu na ni vigumu kuyathibitisha kisayansi. Mfano. suluhisho la umasikini wa nchi zinazoendelea ni kumuomba mungu.

5.    Falsafa; ni mawazo ya busara yenye kutawaliwa na misingi mahususi juu ya asili na maana ya ulimwengu na maisha ya mwanadamu. Falsafa ya mwandishi inaweza kujulikana kwa kusoma kazi zake zaidi ya moja.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne