BANGI NYINGI! KONA NYINGI! GIA NYINGI! MWENDO TU!


Walimuita dereva Kankono! Mkono wa kulia ulipinda kidogo kutokana na ajali kadhaa za gari alizopata kutokana na udereva wake wa pupa! Ila watu walimpenda, walisema, ukipanda gari lake wala makalio hayaumi, sekunde tu, unafika uendako. Waliojaribu kuhoji zaidi waliambiwa kufa kupo tu, kama siku yako imepangwa huwezi kwepa! AKILI NDOGO ZILIFIKIRI KIDOGO.
Jana kabla ya safari, dereva Kankono, alifanya maandalizi ya kutosha. Alianza kwa kuvuta bangi ya miatisa kisha akamalizia kwa kunywa bia saba. Akawa ‘fit’ tayari kabisa kukaa nyuma ya usukani.
Alipoliwasha gari abiria walishangilia! “woyoooooh.” Kankono akafurahi. Haraka sana akakanyaga ‘krach’ akapachika gia ya kwanza, ‘krach’ gia ya pili, ‘krach’ gia ya tatu… mayowe yakaongezeka, Kankono akamaliza gia zote, ‘at their own risk.’
Gari lilikimbia kilomita 117 kwa saa katika barabara mbovu yenye kona nyingi. Kankono hakujali, badala yake akiwa katika mwendo huo, alichukua kilo moja ya mirungi akaanza kutafuna kama beberu la mbuzi. Alipomaliza mirungi, akachukua kikopo cha ugoro, akaanza kwa kunusa, akapiga chafya nene, gari likayumba, watu wakashangilia, “woyooooh.” Akiisha kuachana na kikopo cha ugoro, akaamua kutuliza mawazo yake ili aendelee na safari!

Mara ghafla kona kali, akajitahidi akaikwepa na kuongeza mwendo mpaka kilomita 129 kwa saa! kona ya pili akapita ila gari likalala kidogo, kona ya tatu gari likayumba, kona ya nne gari likaacha njia kisha likagonga mti mkubwa wa mbuyu. NITAKUWA MWONGO NIKISEMA KUNA MTU ALIPONA.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1