Uhakiki wa Diwani ya Chungu Tamu

UHAKIKI WA DIWANI YA CHUNGU TAMU


KITABU; CHUNGU TAMU
MWANDISHI; THEOBALD MVUNGI
MCHAPISHAJI; TPH
MWAKA; 1985
MHAKIKI; DAUD MAKOBA
Chungu tamu ni diwani ambayo inajaribu kupinga dhuluma kwa nguvu zote na kutetea haki za wanyonge. Maudhui yanayoibuliwa yana uhalisia wa moja kwa moja na nchi za kiafrika hususani Tanzania.

Maudhui

Dhamira

1.      Ulanguzi na biashara za magendo

Mwandishi anajadili jinsi ambavyo ulanguzi unachochea dhiki katika jamii. Ulanguzi husababisha bidhaa zikapanda bei na maisha kuwa magumu. Katika shairi la Chanzo ni wenye kauli mshairi anasema,

“mianzo tukiijua, mipango tajipangia,
Kamwe pasiwe na njia, ulanguzi kujirudia,
Iwe tu twahadithia, mithili historia.”

2.      Viongozi wazembe

Hawa ni viongozi ambao husimama katika mikutano na kuwahimiza watu wafanye kazi huku wao wakiendekeza uzembe kwa kulala ofisini na kukesha katika majumba ya starehe. Mshairi anawataka viongozi hawa waongoze kwa mfano. Katika shairi la Wimbo wake hotubani, mshairi anasema,
“cheo kiko mkononi, agizo li mdomoni,
Kila siku yu pombeni, mchana kutwa ndotoni
Wimbo wake hotubani, raia kazi fanyeni.”

3.      Suala la demokrasia

Mshairi anajadili demokrasia ya nchi za kiafrika, anaonesha jinsi ambavyo viongozi wa nchi hizi hawako tayari kuachia madaraka. Watawala hawa wanataka kutawala milele. Migogoro hii ya kukosekana kwa demokrasia ndio inasababisha kutokea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na kukosekana kwa amani. Katika shairi la Kademokrasi katoweka mshairi anasema,
“Barani mabavu yatumika,
Dikteta asijeanguka,
Na majungu pia ayapika,
Udikteta pasi shufaka,
Nasimulia ya Afrika.”

4.      Matabaka

Katika shairi la kitaswira la Chatu na kuku, mwandishi anaonesha matabaka mawili, tabaka la wanaonyonywa (kuku) na tabaka la wanyonyaji (chatu). Shairi hili linalenga kuamsha hisia za wanyonyaji ili kujikwamua toka mikono ya mnyonyaji.
mwandishi amewatumia chatu na kuku kwamba awali wamekuwa wakiishi pamoja lakini mwishowe chatu akaishia kuwala vifaranga wa kuku. Hivyo katika hali ya kawaida chatu na kuku hawawezi kuishi pamoja tangu mwanzo wa dunia, hivyo mwandishi ametumia hivyo lengo kufikisha ujumbe kwa jamii husika kwani ndiyo inayoteseka pale matabaka yanavyozidi kuibuka siku hadi siku.
Babu hakujali swali langu,
Akaendelea kunipasha habari,
Piku alimezwa huku analia,
Dua akawaombea chatu wote,
Mabaya yawafike,
Wapi kuku akamezeka,
Paku akafungwa,
Pangoni akafikishwa.”  

5.      Uzalendo

Shairi la Daktari askari linaonesha jinsi ambavyo Adam alivyomzalendo kwa kuamua kuipigania nchi yake ya Tanzania katika vita vya Kagera. Shairi hili ni chachu kwa vijana wote kuamsha morari wa uzalendo na kuipenda nchi yao, kwani kwa kiasi fulani uzalendo umepungua sana katika jamii.
“Basi sikiliza ..... Paukwa . . !,
Vita vikaja,
Damu zikavuja,
Watu wakatoweka,
Maiti zikanuka,
Mali zikatimka,
Raha ikaaga,
Vijiji vikawa mbuga,
Pema pakawa alama ya uovu,
Mabomu yaliacha makovu”

6.      Mmomonyoko wa maadili

Shairi la Fikra za waungwana linamjadili mwanamke aliyepoteza maadili yake ya asili hata akathubutu kuomba aolewe na wanaume wawili! Suala la mwanamke kuolewa na wanaume wawili ni kinyume na maadili ya Mtanzania. Mshairi anasema,
                        “Mume wangu nakupenda, Joseph amenikuna,
                        Nimekula naye tunda, ninampenda sana,
                        Na usifanye inda, mimi ni wako kimwana,
                        Nitaishi kwa mpango, kwako na kwake Joseph.

7.      Mapenzi

Mwandishi anajadili dhana ya mapenzi katika shairi la Manzese mpaka Ostabei. Mashaka anampenda msichana wa Ostabei Dora, lakini wazazi wake Dora, wanakataa binti yao kuolewa na kijana masikini wa Manzese. Mvutano mkubwa unatokea lakini Dola analazimisha kwa hali na mali lazima awe na Mashaka. Hatimaye wazazi wanakubali na ndoa inafungwa.
Mwandishi anajaribu kuonesha kuwa suala la mapenzi halina ubaguzi bali ni watu kuridhiana na kupendana wa dhati peke.
                        “Hadithi njoo, uende Manzese,
Upite Kariakoo,
Mwisho wako Ostabei,
Mjini Bandarisalama,
Wengine wameliita Jiji…”

Ujumbe

1.      Mapenzi hayachagui chochote ilimradi watu wapendane na kuridhiana.
Ujumbe huu unapatikana katika shairi la Manzese mpaka Ostabei.
2.      Taifa lipige vita na kuwakomesha mara moja viongozi wazembe.
Ujumbe huu umejadiliwa katika shairi la Wimbo wake hotubani.
3.      Demokrasia ni suala lisilokwepeka kwa maendeleo ya jamii yoyote ile
Kama ilivyojadiliwa katika shairi la Kademokrasi katoweka.
4.      Nchi itajengwa na wananchi wenyewe hivyo ni vyema kutengeneza mazingira ya kupata vijana wazalendo walio tayari kulipigania taifa lao.
Kama ilivyojadiliwa katika shairi la Daktari askari.

Migogoro

-          Migogoro ya kisiasa

Viongozi wanang’ang’ania madaraka, wanadhulumu mali ya umma na kunyanyasa watu wanaojaribu kuwapinga. Mgogoro huu unadhihirishwa katika shairi la Kademokrasi katoweka.

-          Migogoro ya kiuchumi

Katika jamii yanaonekana matabaka mawili kinzani, tabaka la wenye nacho na wasionacho. Wenye nacho wanawanyonya na kuwanyanyasa wasionacho na kusababisha mgogoro ambao suluhisho lake si rahisi kupatikana, kama inavyooneshwa katika shairi la Chatu na kuku.

-          Migogoro ya kiutamaduni

Mwanamke anaonekana akipingana na utamaduni wake kwa kudai naye aolewe na wanaume wawili kama jinsi ambavyo mwanaume ana uhuru wa kuwa na wanawake wawili na kuendelea. Mgogoro huu umejitokeza katika shairi la Fikra za waungwana.

Msimamo

Mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi kwani ametoa suluhisho la kupambana pamoja ili kuyaondoa matatizo mbalimbali yanayozikumba nchi za kiafrika. Mwandishi anashauri kurejeshwa kwa demokrasia ili serikali ziwe mali ya ‘umma’ na si mali ya wachache wenye tamaa.

Falsafa

Mwandishi anaamini katika usawa kwa watu wote ili kuleta maendeleo. Mwandishi hafurahishwi hata kidogo na kustawi kwa matabaka ambayo yamepelekea kuwagawa maskini na matajiri.

Fani

Muundo

Msanii ametumia muundo changamano. Hata hivyo mashairi mengi yametumia muundo wa tarbia,  mfano katika shairi la Fikra za waungwana  pamoja na sabilia, mfano katika shairi la Daktari askari.

Mtindo

Mshairi ametumia mitindo yote miwili, yaani wa kimapokeo na wa kisasa.

Matumizi ya lugha

TAMATHALI ZA SEMI
-          Tashibiha
Mweusi kama kiatu cha jeshi (Manzese mpaka ostabei)
-          Tashihisi
Katika ile baridi kali, mabomu ya mikono yakatubusu miguuni (Daktari askari)
-          Sitiari
Ushairi ni sukari tamu (Chungu tamu)
-          Tafsida
Nimekula naye tunda (Fikra za waungwana)
PICHA NA TASWIRA
Chatu – inawakilisha wanyonyaji
Kuku – wanyonywaji
Ngulu – vijiji/jamii iliyosahaulika katika kupatiwa maendeleo
MISEMO NAHAU NA METHALI
-          Lakini haikutiwa chumvi mitaani
-          Kuvaa masulupwete
-          Umoja ni nguvu
-          Sasa mwaleta shari

Kufaulu kwa mwandishi

Amejadili kwa kina matatizo mengi yanayozipata jamii za kiafrika, pia amejaribu kutoa masuluhisho ya matatizo hayo.
Vilevile amefaulu kutumia mitindo yote miwili, kimapokeo na kisasa.

Kutofaulu kwa mwandishi

Baadhi ya mashairi yametumia lugha ngumu ambayo inamfanya kila mhakiki alifasiri shairi kwa mtazamo wake.

TAMATI

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne