KF 202 | Hakiki Madai Kuwa Ushairi wa Kiswahili Hautoki Katika Ombwe au Utupu

Mchoro wa mwanamke akiwa amebeba kibuyu.


Kama ilivyofasiriwa na wataalamu mbalimbali, wakiwemo wana ukale na usasa, tukianza na wanamapokeo, wao wanadai kuwa; ushairi au utenzi ni wimbo hivyo kama shairi halimbiki halina maana. (Amri Abed; 1954).

Shaaban Robert (1958) anasema ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. zaidi ya kuwa sanaa ya vina ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari mawazo, maana na fikra za ndani zinapoelezwa kwa mhtasari wa ushairi huvuta moyo kwa namna ya ajabu.

Nae Mnyampala (1970) anasema ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale. Ndicho kitu bora kwa maongozi ya dunia kwa kutumia maneno ya mkato na lugha nzuri yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa vina na mizani na vina maalumu.

Ubora wa dhana za wana mapokeo ni kwamba; wote wanakubaliana kuwa, ushairi ni lazima uwe na urari wa vina na mizani.

Pia ushairi ni lazima uvute hisia za moyo kutokana na lugha ya kinathari inayotumika. pia ushairi ni wimbo hivyo ni lazima upangwe kwa namna itakayoweza kuimbika. vina na mizani.

Pamoja na ubora wao, wanamapokeo nao wanaonesha udhaifu kwani wameegemea sana katika fani (lugha na kusahau kipengele muhimu cha maudhui) kama tukirejelea fasiri ya Amri Abed. (1954).

Wanausasa nao wamefasiri ushairi kama ifuatavyo; Mulokozi na Kahigi (1982) wanasema ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalumu wa maneno fasaha na yenye muwala kwa lugha ya mkato, picha,, sitiari au ishara katika usemi, maandishi au mahadhi ya wimbo au kueleza tukio a hisi fulani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu wa njia inayogusa moyo.

Njovu na Chimela (1999) wanasema ushairi ni sanaa inayotambulishwa na mpangilio maalumu wa sentensi au vifungu. mpamgilio ambao una muundo maalumu au ruwaza fulani inayounda wizani, lugha ya mkato na mafumbo pamoja na mpangilio usio wa kawaida wa vifungu fulani.

Wizani ni urari wa mapigo ya sauti katika kuongea. Mtu anayezungumza kishairi kidogo hufanana na muimbaji ambaye hupanga maneno yake kufuata mahadhi fulani.

Ubora wa fasili zao ni kwamba, wote wanaona ushairi ni sanaa ya lugha inayopambanuliwa kwa mpangilio maalumu wa maneno fasaha na yenye muwala, lugha ya mkato, picha na sitiari au ishara.

Wamezingatia vipengele vya fani na maudhui kwa kiasi fulani wakiamini kuwa shairi hata lisipoimbika ila likawa na maana na muundo wa kishairi basi hilo linahesabika kuwa ni shairi.

Pia wamechangia kuinuka kwa watunzi wengi wa ushairi wa Kiswahili kutokana na kulegezwa kwa kanuni za utunzi.

Pamoja na ubora wao, wameonekana kuwa dhaifu kwani, mashairi yao yamepoteza utamu na mapigo ya kimuziki.

Hivyo tunaweza kusema kuwa, ushairi ni sanaa ya lugha iliyoandikwa au kuganwa, inayoweza kuwa na urari wa vina na mizani au isiwe nao na inayotumia lugha inayoteka hisia za wasomaji na wasikilizaji. pia tunaweza kusema kuwa ushairi wa Kiswahili ni ushairi uliotungwa na kughanwa unaoelezea utamaduni wa waswahili.

Ni ukweli kwamba ushairi wa Kiswahili hautoki katika ombwe au utupu. Muda na mazingira na tamaduni za waswahili zimechangia sana kuibuka kwa ushairi. Tunaweza kuuweka ukweli huu katik nyakati tofautitofauti na pia kujadili kwa mujibu wa nadharia za wataalamu mbalimbali. tuianza kuthibitisha hoja hizi kwa vipindi mbalimbali.

Ushairi wa Kiswahili kabla ya karne ya 10. Ulikuwa tungo simulizi hasa ngoma na nyimbo. Pia ulifungamana na ngoma za tamaduni za waswahili. Ushairi ulitungwa na kughanwa kwa gibu ila kuandikwa. Pia gibu hii haikufuata urari wa vina na mizani.
Mfano; Nkuli mbondabonde, nkoluti momulyego
             Ndyenyama nkongeigufa nka kiino elya muganga.
ikiwa na maana ya  
            Nikonge na kupinda kama milima ya nyumba za msonge
            Nile nyama na kuiuma mifupa kama jino la muganga. (Richard Mutembei 1993;26)
kipindi hiki ushairi ulighanwa kwa lengo la kusifu au kuiabudu miungu pamoja na shughuli nyingine za kiutamaduni, mfano kuoza binti wanawari.

Ushairi wa Kiswahili kuanzia mwaka 1000 BK. Waswahili waliingiliwa na walowezi kutokea uarabuni nao waliingiliana katika mambo yote ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. kutokana na muingiliano huu waliuathiri ushairi wa Kiswahili kama sehemu ya utamaduni wa waswahili.

Kwanza walileta dini ya kiislamu, iliyoathiri kwa kiasi kikubwa ushairi wa waswahili.

Pili walileta taluma ya uandishi kwa kutumia hati za kiarabu. kutokana na ujio wa waarabu, waswahili nao walianza kushiriki mila na desturi za wageni hao na dini yao. kwa njia hii ujuzi na tabia ama tamaduni za waswahili zilianza kubadilika na hata katika ushairi walianza kutunga mashairi yaliyomsifu Allah na kumuomba baraka.

Pia kati ya mwaka 1000 hadi 1500, miji ya waswahili iliendelea sana kutokana na maingiliano ya kibiashara ambayo iliwaunganisha waswahili wa pwani na bara pia.

Katika kipindi hiki kuliibuka kwa washairi maarufu wa Kiswahili, kama Fumo Lyongo anayeaminika kuishi maeneo ya Pate kaskazini mwa Kenya kama ilivyonukuliwa na Ohly (1985 – 462). Katika kipindi hiki ushairi wa Kiswahili uliendelea kuandikwa na kughanwa ukiwa na maudhui mbalimbali, mfano, “Utenzi wa tawasifu”, na “utenzi wa kumswifu Yanga”. Ambao ndio unasadikika kuwa ndio ushairi wa mwanzo wa Kiswahili kuandikwa mwaka 1517 na ulikuwa na lengo la kumsifu Mwanayanga.

Ushairi wa Kiswahili katika mwaka 1500 – 1750 BK. Kulitokea uvamizi wa wareno katika jamii za waswahili mwaka 1498. Kuliibuka kwa mgogoro baina ya wenyeji na wageni (Wareno) na mashairi yaliandkwa kupinga uvamizi huo. Mojawapo ya mashairi yaliyoandikwa ni “Mzungu Migeli” na “Portugez Afala”. (Hichens;1962.123).

Mbali na mashairi ya kupinga uvamizi wa wareno pia yapo mashairi yaliyoandikwa kuhus maisha ya Mtume Muhammad. Pia upo “Utenzi wa Tambuka” ulioelezea maisha na vita kati y waislamu wa mwanzo na mfalme Herekali wa dola ya Warumi.

Kwa ujumla katika kipindi hiki ushairi uliandikwa kuwatia moyo waswahili na maudhui ya kidini.

Ushairi wa Kiswahili katika kipindi hii ya . ushairi vilevile ulijikita zaidi katika fasihi ya dini na kutafakari maisha kwa ujumla. Kipindi hiki tungo nyingi za maisha ya mtume Muhammad zilitungwa. mfano “Utenzi wa Kiyama” uliokuwa kielezea maisha ya ahera.

Pia kulikuwa na tungo za kiutamaduni. mfano “Utenzi wa Mwanakupona” uliotungwa na Bi Mwanakupona kumhusu bintiye.

Pia katika kipindi hiki jamii kubwa za waswahili zilikuwa katika harakati ya kutafuta uhuru kutoka kwa wakoloni, mashairi mengi yaliandikwa pia. mfano Muyaka bin Haji wa Mombasa, alitunga mashairi kupinga uvamizi wa waarabu wa Oman. Baadhi walinyongwa kwa kukataa kutawaliwa.

Ushairi wa Kiswahili katika karne ya 19. Ulishuhudiwa ujio wa wakoloni katika kipindi hiki.

Wakoloni wa kwanza walikuwa wajerumani ambao walitamalaki 1885 – 1914. Ushairi katika kipindi hiki ulihusu vita vya wenyeji dhidi ya wakoloni wa kijerumani. Mfano “Utenzi wa vita vya Wadachi uliadikwa katika kipindi hiki.

Wajerumani waliacha athari katika ushairi wa Kiswahili ikiwemo; kuanza kutumika kwa hati za kirumi, ufunguzi wa shule, waliosoma walijifunza uandishi wa mashairi, kuanzishwa kwa magazeti, magazeti haya yalikuwa na kurasa maalumu kwa ajili ya mashairi na ni katika kipindi hiki waswahili Shaaban Robert na Mathias Mnyampala waliibuka.

Katika kipindi cha waingereza shule zilimarishwa zaidi na magazeti yaliongezwa zaidi. pia yakaanza kuibuka mashairi ambayo hayakuwa na viwango.

Ushairi wa Kiswahili katika kipindi cha uhuru. kupatikana kwa uhuru kulileta mkondo mpya wa uandishi wa mashairi. Mashairi mengi yakawa ni ya kuwasifu wapigania uhuru. mfano Saadan Kandoro, “Tumshukuru maanani”.

Kipindi cha uhuru pia kilikuwa kipindi cha kuibuka kwa mashairi ya kihakiki ambayo hayakuwa katika mkondo wa kikasuku. mfano Seif Khatib aliandika “Fungate ya Uhuru.”

Katika kipindi hiki pia paliibuka mgogoro wa ushairi kati ya wanausasa na wanamapokeo. Mgogoro huu ni mrefu na unahitaji mjadala wa peke yake. Kwa ufupi tu wanausasa hawakukubali kufungwa na sheri ya urari wa vina na mizani katika shairi.

Ushairi wa Kiswahili katika kipindi cha utandawazi. Utandawazi umeimarika katika kipindi cha miaka ya 1990. umeingiza athari nyingi za kigeni katika ushairi mojawapo ya athari hizo ni kuibuka kwa ushairi mpya kama bongofleva na taarabu.

Hivyo ni kweli kabisa kuwa ushairi wa Kiswahili haukutoka katika ombwe au utupu bali umepitia katika vipindi mbalimbali ambamo ushairi huu umechota mambo na sifa kadha wa kadha. Hata hivyo ushairi wa Kiswahili katika kipindi cha ubepari umebadilika mno, hasa ukizingatia katka kipindi hiki kila kitu huwa ni biashara.

MAREJEO
Samwel. M.(2015). Umahiri Katika Fasihi ya Kiswahili. Mevel Publishers. Dar es salaam

Hyslop, G (1957) Afadhali Mchawi. Nairobi.EALB

Kahigi, KK & M.M Mulokozi (1973) Mashairi ya Kisasa. Dar es salaam: Tanzania Publishing House

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne