Uhakiki wa Riwaya ya Vuta N’kuvute

UHAKIKI WA RIWAYA YA VUTA N’KUVUTE

MWANDISHI: SHAFI ADAM SHAFI
WACHAPISHAJI: MKUKI NA NYOTA
MWAKA: 1999
MHAKIKI: MWALIMU MAKOBA

Utangulizi

Vuta n’kuvute ni riwaya inayozungumzia mvutano uliopo baina ya wakoloni na watawaliwa vilevile inaonyesha msuguano na mvutano uliopo kati ya wazazi na watoto katika suala la mapenzi.

Maudhui

DHAMIRA
UKOMBOZI
Mwandishi anaonyesha aina mbalimbali za ukombozi unaohitajika katika jamii. Mfano: ukombozi wa kiutamaduni. Hapa anapinga mila zinazomkandamiza mwanamke. Kwa mfano, Yasmini kulazimishwa kuolewa na Raza, ni unyanyasaji usiokubalika.
Pia, ukombozi wa kisiasa. Mwandishi anaonyesha jinsi ambavyo Zanzibar ilitawaliwa na Waingereza. Wahusika Denge na wenzake wanapambana vilivyo kuhakikisha uhuru wa Zanzibar unapatikana.
Ukiachilia mbali aina hizo mbili za ukombozi, mwandishi pia amejadili ukombozi wa kiuchumi na fikra.

Mapenzi

Mwandishi anajadili mapenzi ya kweli na yale ya uongo. Katika mapenzi ya kweli, Mwajuma, Denge na kundi lake wanamapenzi ya kweli kwa jinsi walivyopendana wao kwama marafiki na jinsi walivyoipenda nchi yao.

Matabaka

Matabaka matatu yanaonekana:
-      Wazungu. Hawa waliheshimiwa kuliko matabaka yote. Wazungu wanawakilishwa na wahusika kama, Inspekta Wright.
-      Wahindi. Hawa walifuata baada ya tabaka la wazungu. Wahindi wanawakilishwa na wahusika kama, Raza, Gulamu na wengine wengi.
-      Waafrika. Hawa hawakuheshimiwa, walibaguliwa na kunyanyaswa. Waafrika wanawakilishwa na wahusika kama Denge, Mwajuma, Koplo Matata, Mambo, Sukutua n.k

Nafasi ya mwanamke katika jamii

Mwanamke amechorwa katika nafasi mbalimbali:
-      Kiumbe duni asiye na maamuzi yoyote. Yasmini analazimishwa kuolewa na mwanamume asiyempenda kwa sababu tu alionekana duni na siyeweza kutoa maamuzi.
-      Mwenye upendo wa kweli. Mwajuma alimpenda Yasmini hata akakubali waishi wote bila kujali fikra za utabaka na ubaguzi wa rangi uliotawala.
-      Mwanamapinduzi asiyependa mila zilizopitwa na wakati. Yasmini anaamua kuondoka kwa mumewe, mwanamume ambaye alimuoa pasi na ridhaa yake. Msichana huyu anaamua kutafuta uhuru wake mwenyewe.
-      Chombo cha starehe. Yasmini anatumika kumstarehesha Denge. Naye Mwajuma anatumika kumstarehesha Mambo.

Ujumbe

i.             Suala la mapenzi lisiingiliwe na wazazi. Ni vyema maamuzi ya yupi wa kuoa/kumuoa wakaachiwa wale tu wanaopendana. Yasmini anashindwa kuishi na Bwana Raza kwa sababu hakumpenda.
ii.            Ukombozi wa Afrika unahitajika kwa gharama yoyote ile. Waafrika wote waungane ili kuweza kupambana na ukoloni mamboleo na aina nyingine za ukoloni ambazo zinarudisha nyuma maendeleo ya bara hili.
iii.           Ukoloni si jambo jema. Mateso wanayopata akina Denge na wananchi wengine yanauchora waziwazi uovu na ubaya wa ukoloni.
iv.          Elimu inahitajika katika jamii. Ni wakati sasa jamii inapaswa ipatiwe elimu ili iweze kupambana na kuwa huru katika matatizo mbalimbali.

Migogoro

Migogoro ya wahusika
-      Yasmini na Raza
-      Yasmini na wazazi wake
-      Yasmini na Bukhet
-      Denge na Koplo Matata
-      Denge na Koplo Matata
-      Denge na Inspekta Wright

Migogoro ya nafsi

-      Yasmini. Anapatwa na mgogoro wa nafsi pale anapoolewa na mtu asiyempenda. Suluhisho la mgogoro huu ni Yasmini kumkimbia mumewe.
-      Bukheti. Anampenda sana Yasmini, anapata mgogoro wa nafsi endapo kama Yasmini ataweza kumwelewa nakumkubalia ombo lake. Suluhisho la mgogoro huu ni Bukheti kuamua kusafiri mpaka Zanzibar. Hatimaye anafanikiwa kumuona Yasmini.

Migogoro ya kiuchumi

Wananchi wakiwakilishwa na Denge, wanataka uchumi wao urejeshwe katika mikono yao wenyewe. Wanachukia uchumi wa nchi yao kushikiliwa na wakoloni.

Migogoro ya kisiasa

Wananchi wa Zanzibar wanataka utawala wao wenyewe. Wamechoka kutawaliwa na wakoloni. Mgogoro huu haupati suluhisho mpaka mwisho.

Mgogoro wa kiutamaduni

Vijana wako kinyume na tamaduni walizozikuta. Tunamuona Yasmini akikataa kuishi na mumewe Raza ambaye hakumpenda.

Msimamo

Msanii ana msimamo wa  kimapinduzi, kwani anaamini kuwa, suala la ukoloni na tamaduni zinazomkandamiza mwanamke linaweza kuondolewa kwa kuungana pamoja na kupambana.

Falsafa

Mwandisi anaamini kuwa, ukoloni utaondolewa kwa kuungana pamoja na kupambana.

Fani

Muundo

Mwandishi katumia muundo wa moja kwa moja. Anasimulia maisha ya Yasmini na Denge moja kwa moja.
Anaanza masimulizi kwa kumuonyesha Yasmini katika ndoa, Yasmini anatoroka, kisha anakutana na Denge. Pia, anaonyesha harakati za Denge kupigania ukombozi, anavyofungwa jela na anapotoka.

Mtindo

Mwandishi ameiwasilisha kazi yake kwa kutumia mtindo wa:
-      Monolojia. Hii ni lugha ya masimulizi katika kazi ya fasihi.
-      Dayolojia. Hii ni lugha ya majibishano.
-      Barua. Yasmini alimuandikia barua mpenzi wake Denge.
-      Nyimbo. Kikundi cha taarabu kilichoitwa cheusi dawa kilitumbuiza nyimbo mbalimbali. Yasmini na Mwajuma nao waliimba taarabu palipotokea shughuli.

Matumizi ya lugha

Matumizi ya lugha hujikita katika vipengele vitatu:
-      Tamathali za semi
-      Misemo, methali na nahau
-      Picha na taswira

Tamathali za semi

Tashibiha.
“Bwana Raza amekaa juu ya kiti amevimba kama kiboko.”
“Mweupe kama mgonjwa wa safura.”
Tashihisi
“Nuru ya jua iliingia wa hamaki chumbani mule na ilikashifu uchafu wote wa chumba kile.”
Takriri
“Yeye hakuona isipokuwa Yasmini, Yasmini, Yasmini gani naye?”
“Haya tunywe, tunywe kwa afya ya mgeni wetu.”
Mjalizo
“Kula mkate wa ufuta, mkate wa maji, mkate wa mayai.”
Tanakali sauti
“Ngo! Ngo! Ngo!”

Misemo, Methali na Nahau

“Hujui kama mkono wa serikali ni mrefu.”
“Kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa.”
“Heri nusu shari kuliko shari kamili.”

Picha na taswira

“Yasmini alikuwa na kijiuso kidogo, macho makubwa, pua ndogo na nyembamba, alikuwa na nywele nyingi.”
Matumizi ya lugha ya picha
Komunisti – hili ni jina ambalo waliitwa waafrika waliojitolea kupigania uhuru kama Denge.

Wahusika

YASMINI
-      Mwanamke asiyependa tamaduni kandamizi. Anamtoroka mumewe na kwenda kuolewa na mwanamume anayempenda.
-      Mvumilivu. Anayavumilia maisha magumu anayokutana nayo kwa Mwajuma.
-      Ana upendo wa kweli. Anampenda kwa dhati mpenzi wake Denge.
DENGE
-      Mwanaharakati na anayepinga utawala wa mwingereza kisiwani Zanzibar.
-      Kijana aliyesoma Urusi na anaitumia vyema elimu yake.
-      Anampenda Yasmini na wanafanikiwa kupata mtoto mmoja.
MWAJUMA
-      Rafiki yake Yasmini
-      Ana upendo wa kweli
-      Mwanachama wa kikundi cha ‘cheusi dawa.’
-      Anapenda pesa
Wahusika wengine ni: Koplo Matata, Chande, Sukutua, Raza, Salehe, Wright, Shihab na Bukhet.

Mandhari

Mandhari yaliyotumika yamegawanyika katika miji hii:
-      Unguja
-      Tanga
-      Mombasa
-      Dar es Salaam
Vilevile kuna mandhari ya:
-      Dukani
-      Gerezani
-      Baharini
-      Nyumbani
-      Mitaani
-      Baa
-      Klabu

Kufaulu kwa mwandishi

-      Amefanikiwa kuonyesha mvutano wa wazazi na watoto wao.
-      Ametumia lugha nzuri iliyopambwa kwa tamathali nyingi za semi.

Kutofaulu kwa mwandishi

-      Suluhisho la mgogoro wa wakoloni na watawaliwa halijatolewa na mwandishi.

-      Mwandishi hajaonyesha mipaka ya uhuru inayotakiwa na watoto. Mfano: Yasmini anaolewa na mwanamume anayempenda, Shihab. Lakini ndoa yao inashindwa kudumu.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne