Maajabu ya Mugabe, Maajabu ya Umoja wa Afrika
Robert Mugabe, baba wa taifa la Zimbabwe
amepita katika nyakati nyingi kinzani. Kwanza, akiwa kama shujaa, mkombozi wa
nchi yake kutoka kwa mkoloni. Pili akiwa mtetezi wa wanyonge weusi,
aliyethubutu kuwanyang’anya mashamba wazungu na kuwapatia wazawa. Hili la tatu
linasababishwa na jambo la pili, Mugabe akiwa madarakani anashuhudia nchi
ikiporomoka kwa kasi ki uchumi, mporomoko huo unaifanya nchi hiyo ishindwe hata
kutumia fedha yake!
Umoja wa mataifa ya Afrika haukuisaidia
Zimbabwe katika masaibu haya. Masaibu ambayo ama kwa hakika yamesababishwa na
mataifa ya kibeberu. Umoja huu butu utawezaje kuisaidia Zimbabwe ikiwa umoja
huu asilimia 60 ya bajeti yake unategemea fedha za msaada kutoka hukohuko
katika mataifa ya kibeberu!
Maajabu ya Umoja wa Afrika hayakuanza zama
hizi, mwaka 1978 ulishindwa kuzuia vita vya Tanzania na Uganda. Na mpaka wakati
huu ukitazama yanayotokea Sudan, Congo, Afrika ya Kati, Nigeria, Somalia,
Libya… lazima ujiulize ni nini hasa kazi ya Muungano wa Afrika – Muungano usio
na fedha…FEDHEHA!
Wiki kadhaa zilizopita, mzee Mugabe akiwa na
mapenzi ya dhati na muungano huu usio na meno, aliamua kuuchangia kidogo
alichojaliwa, mabepari wamebomoa uchumi wa nchi yake kwa kisingizio cha
demokrasia, angetoa nini ikiwa fedha hakuna? Basi mzee wetu alitoa ng’ombe!
Utoaji huu una maana kubwa, kwamba hakuna mwanadamu anayehitaji fedha kwa
hakika, bali twahitaji vitu fulani ambavyo pengine vyaweza kupatikana kwa
urahisi palipo na fedha. Hivyo bara la Afrika kushindwa kuendelea kwa
kisingizio kuwa halina fedha ni UJUHA.