KINACHOENDELEA TANZANIA NA HATMA YETU
“Kumbadili Waziri, hata
waziri mkuu, si jambo la ajabu. Anaweza kujiuzulu, anaweza kufukuzwa na nchi
isitikisike. Lakini huwezi kumtikisa Rais wa nchi bila kuitikisa nchi yenyewe.”
(Nyerere, 1994:59-60).
Sisi kama wananchi wa
kawaida, tunatakiwa kuwachagua viongozi wetu kwa uangalifu mkubwa,
wakishachaguliwa wanatakiwa wajiheshimu na kuwa waangalifu sana. Hapana shaka
Nape hakuwa mwangalifu alipopitisha sheria mbovumbovu ikiwemo kuwanyima wananchi
haki ya kutazama bunge mubashara. Japo anastahili pongezi kwa uungwana
aliouonesha dakika za mwisho. Hali hii ni ya kawaida kabisa kama asemavyo
Jenerari ulimwengu kuwa viongozi wa kiafrika hupata akili wanapomaliza muda wa
utawala wao.
Haya yanatufundisha kuwa
kumbadili waziri si jambo la ajabu, mfano, hayati Mfaume Kawawa alikuwa waziri
mkuu kwa muda mrefu. Hakuwa amefanya kosa lolote, lakini nafasi yake
ilichukuliwa na hayati Edward Moringe Sokoine. Watu aina ya Kawawa hawapatikani
kama pipi dukani, ni watu adimu na huenda huzaliwa kila baada ya miaka 100.
HATMA YETU
Viongozi wabadili mbinu,
jamii imebadilika… lengo letu sote ni lilelile kuiona Tanzania ikisonga mbele
kama farasi wa vita. Kwanza viongozi waepuke kuahidi mambo makubwa ambayo
hawawezi kuyatimiza. Waliahidi huduma bora za kiafya, badala yake tuna vijana
madaktari waliofaulu vizuri zaidi ya 2500 wako mtaani hawana ajira, serikali
haina fedha! huku tukiwa na upungufu wa madaktari zaidi ya 3000. Suala la
walimu na sekta nyinginezo ni ukakasi sasa kulisema.
Viongozi waepuke kutoa
matamko bila kushirikisha wananchi. “Nchi hii si ya kisultani, tukianza
kuvumilia masultani wa kuchaguliwa tutapanda mbegu ya masultani wa kuzaliwa.”
(Nyerere, 1994:59).
Tumeshuhudia viongozi
wetu wakiponzwa na matamko yao wenyewe, na wengine wakizozana na kupingana
hadharani mithili ya kikundi cha wasutaji kilichombana mwongo uchochoroni.
Mwandishi Carnegie, (1936)
anashadadia hoja yangu, “People are more likely to accept an order if they have
had a part in the decision that caused the order to be issued.”
Mwisho viongozi walinde
sura za wanachi wao, si vyema kuwatangaza, kuwatumbua wala kuwananga mchana
kweupe mbele ya kundi kubwa la watu, tuitane kimyakimya, tufuate sheria,
mharifu huwa haitwi mbele ya kamera zilizotangulizwa na matumbo ya waandishi wa
habari. Huo ni uchuro, na matokeo ya vitendo hivi wote tumeyaona. NCHI
IMETIKISIKA KWA KUIBULIWA KASHFA NZITO ZA VIONGOZI ZILIZOKOSA MAJIBU.